Wednesday 14 March 2012

Maelezo Ya Qur’an Kuhusu Bahari Na Mito

Wanasayansi wa zama hizi wamegundua kuwa mahali ambapo bahari mbili tofauti hukutana, kuna kizuizi baina yake. Kizuizi hiki huzigawa bahari mbili hizo kiasi kwamba kila bahari huwa na joto lake, kiwango cha chumvi na msongamano.[1]  Kwa mfano, maji ya bahari ya Mediterranean ni yenye uvuguvugu, yana chumvi na msongamano mdogo yakilinganishwa na maji ya bahari ya Atlantiki. Pindi maji ya Mediterranean yaingiapo Atlantiki katika kizingiti cha Gibraltar, huingia mamia kadhaa ya kilomita ndani ya Atlantiki katika kina cha kadiri ya mita 1000 yakiwa pamoja na sifa zake za uvuguvugu, kiwango uchumvi na uchache wa msongamano. Maji ya Mediterranean huimarika katika kina hiki[2] (Angalia Mchoro: A)

Mchoro: A 
Mchoro A: Maji ya bahari ya Mediterranean yanavyoingia Atlantiki kupitia kizingiti cha Gibraltar yakiwa na sifa yake ya uvuguvugu, uchumvi na msongamano, kwa sababu ya kizuizi kinachoyatofautisha. Kipimo cha joto ni katika nyuzi joto za Selisiasi (Co). (Marine Geology, Kunen, uk. 43, kukiwa na kuweka nyongeza kidogo)

Ingawa kuna mawimbi makubwa, mikondo yenye nguvu na kupwa na kujaa katika bahari hizi, hazichanganyiki wala kuvuka kizuizi hiki.
Qur’an ilieleza kuwa kuna kizuizi baina ya bahari mbili, hazichupi mipaka. Allaah amesema: “Anaziendesha bahari mbili zikutane; Baina yao kipo kizuizi, zisiingiliane.”
Qur’an Surat Arrah'man 55:19-20
Lakini pindi Qur’an inapozungumzia kigawanyi baina ya maji baridi na ya chumvi, hutaja kuwepo kwa “kitenganishi kizuiacho” na kizuizi pamwe.
“Naye Ndiye Aliyezipeleka bahari mbili, hii tamu mno, na hii ya chumvi chungu. Na akaweka baina yao kinga na kizuizi kizuiacho.”
Qur’an Surat Al Furqan 25:53

Mtu anaweza kuuliza, kwa nini Qur’an imetaja kitenganishi pindi izungumziapo chenye kugawanya baina ya maji baridi na ya chumvi, lakini haikukitaja wakati inapozungumzia juu ya chenye kugawanya kati ya bahari hizi mbili?
Sayansi ya zama hizi imegundua kuwa katika milango wa mto ambapo maji baridi (matamu) na maji chumvi hukutana, hali kwa namna fulani ni tofauti na kinachopatikana mahali ambapo bahari mbili hukutana. Imegundulika kwamba kinachotofautisha maji baridi na maji chumvi katika milango bahari ni “ukanda wa pycnocline kukiwa na alama ya kutokukuwepo muendelezo wa msongamano unaotenganisha baina ya tabaka mbili."[3]  Kitenganishi hiki (ukanda wa utengano) una uchumvi ulio tofauti na maji baridi na maji chumvi[4](Angalia Mchoro B).

Mchoro B
 
Mchoro B: Sehemu iliyokatwa kwa urefu ikionesha uchumvi (semu moja kati ya elfu 0/00 katika mlango bahari. Hapa tunaweza kuona kitenganishi (ukanda wa utengano) baina ya maji baridi na ya chumvi. (Introductory Oceanography, Thurman, uk. 301, kukiwa na nyongeza kidogo)

Maelezo haya yamegundulika hivi karibuni tu, kwa kutumia vifaa vilivyoendelea sana kwa kupima joto, uchumvi, msongamano na kuyeyuka kwa oksijeni, n.k. Jicho la mwanaadamu haliwezi kuona tofauti iliyopo baina ya bahari mbili zenye kukutana. Halikadhalika, jicho la mwanaadamu haliwezi kuona mgawanyo wa maji katika milango bahari katika namna tatu: maji baridi, maji chumvi, na kitenganishi (ukanda wa utengano).
__________
[1] Principles of Oceanography, Davis, uk. 92-93
[2] Principles of Oceanography, Davis, uk. 93
[3] Oceanography, Gross, uk. 342. Pia angalia Introductory Oceanography,Thurman, uk. 300-301
[4] Oceanography, Gross, uk. 244. Pia angalia Introductory Oceanography,Thurman, uk. 300-301

No comments:

Post a Comment

Qur'an 5:32